MSIMU WA MAUZO YA KOROSHO NCHINI WA MWAKA 2019/2020 WAFUNGULIWA RASMI

Mhe. Omary Mgumba (Mb), Naibu Waziri Wizara ya Kilimo, akihutubia kwenye Mkutano mkuu wa wadau wa Tasnia ya Korosho nchini uliofanyika Mkoani Mtwara

 • Naibu Waziri Mhe. Omary Mgumba azungumza hayo kwenye Mkutano mkuu wa wadau wa Tasnia ya Korosho
 • Msimu mpya wa mauzo ya Korosho wa mwaka 2019/20 umefunguliwa rasmi na Mhe. Omary Mgumba (Mb), Naibu waziri wa Kilimo kwenye Mkutano mkuu wa wadau wa tasnia ya Korosho uliofanyika Jumatatu tarehe 07 Oktoba kwenye ukumbi wa Mikutano wa Benki kuu Tanzania mkoani Mtwara

  Katika mkutano huo mkuu wa wadau wa tasnia ya Korosho nchini Tanzania Mhe. Mgumba ametangaza kuwa Serikali itawalipa wakulima wa Korosho TSh. 59 bilioni kabla ya Novemba 2019

  Akizungumza leo Jumatatu Oktoba 7, 2019 wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa korosho mkoani Mtwara, amesema katika msimu huo walikusanya korosho tani 222,000 zilizokuwa na thamani zaidi ya Sh722 bilioni na kwa sasa baadhi ya wakulima wanaidai serikali Sh 59 bilioni.

  “Mpaka sasa tumeshalipa zaidi ya 663 bilioni bado kuna wakulima wanadai zaidi ya Sh59 bilioni na tunafahamu kuna zaidi ya Sh24 bilioni za watoa huduma wanadai. Niwahakikishie wadau wote wanaoidai Serikali mpaka kufikia Oktoba 30, 2019 watakuwa wamelipwa,” amesema Mgumba

  Mgumba amesema katika msimu wa 2017/18 zao hilo liliingizia Taifa Sh1.3 trilioni ikiwa ni fedha nyingi kuliko zilizopatikana katika mazao ya kahawa, pamba na madini.

  Aidha ametolea ufafanuzi wa taarifa zinazosambazwa kwamba Serikali itanunua tena korosho msimu wa mwaka 2019/20 na kusema haina nia hiyo na endapo bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko itanunua zao hilo itanunua kama wanunuzi wengine wote.

  Amesema katika msimu wa mwaka 2019/20 wanatarajia kuzalisha zaidi ya tani 290,000 na kwamba maandalizi yote yamekamilika