CBT YAENDELEA KUTOA ELIMU NA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WAKULIMA WA KOROSHO NANENANE - MOROGORO
Morogoro
Banda la Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea mkoani Morogoro limeendelea kuwa kitovu cha utoaji wa elimu, ushauri wa kitaalamu na utatuzi wa changamoto zinazowakabili wakulima wa korosho kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Kupitia maonesho hayo, wakulima wanapata fursa ya kujifunza mbinu bora za uzalishaji, matumizi sahihi ya pembejeo na huduma mbalimbali zinazotolewa na CBT kwa lengo la kuongeza tija katika uzalishaji wa korosho.
Miongoni mwa waliotembelea banda hilo ni ndg. James Chimais mkulima kutoka kata ya Mikumi Wilaya ya Kilosa, ambaye ameeleza kufurahishwa na elimu aliyoipata kuhusu kilimo cha korosho. Aidha, ameeleza juu ya changamoto mbalimbali zinazomkabili katika uzalishaji wa zao hilo, ikiwemo kukosa mashine ya kupulizia mikorosho.
Akijibu hoja hizo, Kaimu Meneja wa CBT mkoa huo, Jafari Matata amempongeza mkulima huyo kwa hatua ya kufika banda la taasisi kutafuta elimu na ufumbuzi wa changamoto zake. Vilevile ameahidi kumtembelea shambani kwake ili kujionea hali halisi na kutoa ushauri wa kitaalamu utakaosaidia kuboresha uzalishaji na kuongeza tija katika uzalishaji sambamba na utaratibu wa upatikanaji wa mashine hiyo.