Skip to main content
CBT YATOA TAARIFA YA MWENENDO WA MINADA YA KOROSHO BAADA YA WIKI MBILI ZA MWANZO MSIMU WA MAUZO 2026/2027
27 Oct, 2026
admin
Habari na Matukio

CBT YATOA TAARIFA YA MWENENDO WA MINADA YA KOROSHO BAADA YA WIKI MBILI ZA MWANZO MSIMU WA MAUZO 2026/2027

MTWARA

Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) imetoa taarifa kuhusu mwenendo wa minada ya korosho ghafi nchini katika wiki mbili za mwanzo kwenye msimu wa mauzo mwaka 2026/2027.

Katika minada hiyo iliyofanyika kwa wiki hizo mbili jumla ya tani 112,303 za korosho ghafi zimeuzwa kupitia minada 10 iliyofanyika kuanzia Oktoba 12, 2026 hadi Oktoba 25 mwaka huu zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 300.

Aidha katika minada hiyo bei ya juu iliyofikiwa kwa korosho daraja la kwanza ilikuwa Shilingi 3,430 huku bei ya chini ikiwa Shilingi 2,970 kwa kilo.

Akizungumza na vyombo vya habari mkoani Mtwara Oktoba 26 mwaka huu, Mkurugenzi Mkuu wa CBT Francis Alfred amesema bodi itaendelea kusimamia mwenendo wa minada ili kuhakikisha taratibu za uuzaji wa korosho zinafuatwa.

Pia uwazi unaimarishwa na ubora wa zao unazingatiwa lengo ni kulinda maslahi ya wakulima na wadau wengine wa tasnia ya korosho nchini.

Mbali na hilo amewahimiza wakulima kuwa na subira na kuendelea kutumia mfumo wa stakabadhi za ghala unaolenga kuwawezesha kuuza korosho zao kwa utaratibu unaotambulika na kuwezesha usimamizi wa mauzo kwa uwazi.

Pia CBT inaendelea kuwakumbusha wakulima kuzingatia uvunaji kwa wakati, ukaushaji wa kutosha na uhifadhi sahihi wa korosho ili kudumisha ubora wa korosho hatua itayosaidia kulinda thamani yake sokoni, pia kuongeza ushindani wa korosho ya Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Lebo: