BODI YA KOROSHO TANZANIA KUCHUKUA HATUA DHIDI YA WABANGUAJI WANAOKIUKA TARATIBU
MTWARA
Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) imewaonya wabanguaji wanaokiuka taratibu za ununuzi wa korosho katika soko la awali, ikisema kuwa itachukua hatua dhidi ya wote wanaokiuka masharti hayo kwa kuwa vitendo hivyo vinaathiri maslahi ya wakulima na kuvuruga mfumo wa biashara ya zao hilo.
Katika hatua ya kukabiliana na ukiukwaji huo, CBT imechukua hatua dhidi ya kampuni moja kwa kuinyima kibali cha kununua korosho, baada ya kudaiwa kuchukua, kubangua na kuuza korosho za wakulima bila kuwalipa kwa wakati.
Mkurugenzi Mkuu wa CBT, Francis Alfred, amesema baadhi ya kampuni zimekuwa zikichukua korosho za wakulima bila kufanya malipo kwa wakati, kinyume na taratibu za soko la awali zinazomtaka mnunuzi kulipa fedha za korosho pamoja na tozo husika kabla ya kuchukua mazao.
Akizungumza katika mahojiano maalumu, Alfred amesema baadhi ya wabanguaji wamekuwa wakitumia ushawishi kwa viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika (Amcos) ili kupata korosho kupitia makubaliano yasiyo rasmi, hali inayoweza kusababisha wakulima kucheleweshewa malipo yao.
“Baadhi ya kampuni hazifuati utaratibu, wanakwenda kuchukua korosho za wakulima, halafu wanawaambia watalipa baadaye. Wakati utaratibu wa soko la awali unasema hutakiwi kuchukua korosho za wakulima bila kulipa,” amesema.
Amesema kampuni hiyo, ambayo hakuitaja jina, imezuiwa kufanya shughuli za ununuzi katika vituo baada ya kubainika kuwa ilichukua korosho za wakulima, kuzibangua na kuziuza bila kuwalipa.
Alfred amesema CBT haijabadilisha utaratibu wa soko la awali, bali inaendelea kusimamia utekelezaji wa masharti yaliyowekwa na Serikali kwa lengo la kuhakikisha biashara ya korosho inafanyika kwa uwazi na maslahi ya mkulima yanalindwa.
WABANGUAJI KUTUMIA MAWAKALA WALIOSAJILIWA
Katika hatua nyingine, CBT imeanza kufuatilia matumizi ya mawakala katika ununuzi wa korosho, huku ikisisitiza kuwa mawakala hao wanapaswa kusajiliwa na kutambulika rasmi na Bodi.
“Kwa wale ambao wangependa kutumia mawakala kununua korosho, tunataka mawakala hao wasajiliwe na Bodi ya Korosho Tanzania. Hatutaruhusu mbanguaji atumie wakala ambaye hajasajiliwa,” amesema Alfred.
Amesema matumizi ya mawakala wasiotambulika yanaweza kufanya iwe vigumu kutofautisha kati ya mawakala halali, kangomba na wanunuzi wengine, jambo linaloweza kusababisha vurugu katika vituo vya ununuzi.
CBT KUIMARISHA UDHIBITI WA MIZIGO
Aidha, CBT imepanga kuimarisha udhibiti wa mizigo ya korosho kabla haijaondoka katika wilaya husika, kwa kuwaweka maofisa katika vituo maalumu vya uhakiki.
Kwa mujibu wa Alfred, maofisa hao watakuwa na jukumu la kuthibitisha kiasi cha korosho pamoja na uhalali wa vibali kabla ya mizigo kusafirishwa.
Hatua hiyo inalenga kudhibiti ukwepaji wa tozo na kuhakikisha kuwa kiasi cha korosho kinachosafirishwa kinaendana na vibali vilivyotolewa.
TAPC YATAKA SEKTA YA UBANGUAJI KUKUZA AJIRA
Wakati CBT ikichukua hatua hizo, Chama cha Wabanguaji Korosho nchini (TAPC) kimeiomba Serikali kuweka mikakati zaidi ya kukuza sekta ya ubanguaji wa korosho, kikisema bado inakabiliwa na changamoto zinazokwamisha ukuaji wake.
Mwenyekiti wa TAPC, Sosthenes Mayoma, amesema sekta hiyo inalenga kuongeza ajira kutoka takribani 14,000 zilizopo sasa hadi 50,000 ifikapo mwaka 2030.
Mayoma amesema ili kufikia lengo hilo, Serikali inapaswa kuwawezesha wabanguaji kwa kuondoa vikwazo vinavyoikabili sekta hiyo na kuongeza uwekezaji katika shughuli za ubanguaji wa korosho nchini.
Kwa upande wake, Farida Juma, mbanguaji kutoka Newala, amesema kuwawezesha wabanguaji wadogo kupata teknolojia na vifaa vya kisasa kutasaidia kuongeza uzalishaji na ushindani katika soko.
Amesema ukosefu wa teknolojia na vifaa vya kisasa ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili sekta hiyo, akisisitiza kuwa mafunzo pamoja na upatikanaji wa nyenzo bora vinaweza kuongeza ufanisi wa uzalishaji.
Sekta ya ubanguaji wa korosho inaelezwa kuwa na uwezo mkubwa wa kutoa ajira zaidi ya 100,000, hususan kwa wanawake na vijana, endapo uwekezaji utaongezeka na mazingira rafiki ya biashara yataimarishwa.