MKURUGENZI MKUU CBT AITAKA KOROSHO QUEENS KUENDELEA KUWA BALOZI WA TASNIA YA KOROSHO
MTWARA
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Francis Alfred ameeleza kuridhishwa na kazi inayofanywa na wachezaji wa timu ya mpira wa wavu ya Korosho Qeens inayofadhiliwa na Bodi ya Korosho Tanzania.
Akizungumza katika Ofisi za Bodi ya Korosho Tanzania Mtwara Septemba 3, 2026, wakati timu hiyo ilipofika ofisini kwake kwa ajili ya kukabidhi kombe la MUUNGANO ambalo Korosho Queens ndio BINGWA kwa msimu wa 2026 uliofanyika Zanzibar, ameitaka timu hiyo kuendelea kuwa balozi wa tasnia ya korosho kwa kuitangaza tasnia, kuhamasisha ulaji wa korosho, ubanguaji, pamoja na matumizi ya bidhaa zitokanazo na zao la korosho.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu ameunga mkono jitihada zinazofanywa na timu hiyo na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano ili kuiwezesha kufanya vizuri zaidi katika mashindano yake sambamba na kuwataka viongozi na wachezaji wa timu hiyo kuhakikisha wanatumia fursa ya michezo kujenga maisha na mustakabali mzuri wa baadaye.
Amesisitiza kuwa timu hiyo inapaswa kuendelea kufanya vizuri katika mashindano ili kuwa chachu ya kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kula korosho kwa afya, sambamba na kuongeza uelewa kuhusu faida za zao hilo.
Kwa upande wake, Meneja wa timu hiyo, Ndugu Hussein Kibombwe, amesema kauli mbiu ya “Kula Korosho kwa Afya” imeendelea kuwa na matokeo chanya kwa wadau na mashabiki wa timu hiyo katika maeneo mbalimbali.
Timu hiyo imeendelea kutumia nafasi mbalimbali za michezo na matukio yake kuitangaza tasnia ya korosho, bidhaa zitokanazo na zao hilo pamoja na kuhamasisha jamii kuhusu ulaji wa korosho kwa afya.