Skip to main content
TANZANIA YAWEKA MKAKATI WA KUONGEZA UZALISHAJI WA ZAO LA KOROSHO
27 Aug, 2026
admin
Habari na Matukio

TANZANIA YAWEKA MKAKATI WA KUONGEZA UZALISHAJI WA ZAO LA KOROSHO

MOROGORO

Tanzania imeweka mkakati wa kuongeza tija na ubora wa zao la korosho kwa lengo la kufikia uzalishaji wa tani milioni moja ifikapo mwaka 2030 na kushika nafasi ya kwanza kwa uzalishaji wa korosho barani Afrika.

Hayo yamesemwa na Mhe. Adam Malima, aliyemwakilisha Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb), katika Mkutano Mkuu wa Wadau wa Tasnia ya Korosho Nchini unaofanyika Agosti 27, 2026 katika Hoteli ya Morena, Morogoro.

Mhe. Malima amesema kufikia azma hiyo kunahitajika ushirikiano wa wadau wote katika mnyororo wa thamani wa korosho, huku akiwataka wakulima, wafanyabiashara, wabanguaji, Serikali na taasisi za utafiti kuongeza kasi ya uzalishaji na kuzingatia ubora wa zao hilo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania,Ndg. Francis Alfred, amesema mkakati wa Serikali unaelekeza katika kuongeza tija ya uzalishaji, aidha ameeleza kuwa upatikanaji wa mbegu bora zenye uwezo wa kustahimili visumbufu, magonjwa na mabadiliko ya hali ya hewa ni muhimu katika kuongeza uzalishaji, akisisitiza juu ya mchango wa tafiti zinazofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI). 

Mkutano huo uliwakutanisha pamoja viongozi wa Serikali, akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Prof. Peter L. M. Msoffe, Wakuu wa Mikoa na Wilaya zinazolima zao la Korosho, Wabunge, wakulima, wanunuzi, wabanguaji, vyama vya vikuu vya ushirika, taasisi za kifedha na wadau wengine katika mnyororo wa thamani wa zao la korosho.

Lebo: